Imechapishwa: Oct 17, 2024 17:47
Reference No: TZCERT-NEW-24-0002
Katika zama za taarifa na uchumi wa kidijiti, ambapo kila kitu kutoka masuala ya benki hadi burudani hufanyika mtandaoni, usalama mtandaoni ni muhimu zaidi kuliko hapo awali. Kadiri taifa linavyokumbatia mabadiliko ya kidijitali, na kuongezeka kwa watumiaji wanaounganishwa mtandaoni, huduma salama za mawasiliano suala la msingi hasa katika kutengeza mtandao ulio salama kwa wote. Kulinda rasilimali zetu za dijitali ni muhimu kuhakikisha usalama wa watu binafsi, biashara, na taifa kwa ujumla. Kama Doreen Bogdan-Martin, Katibu Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Dunia (ITU), alivyosema, "Kujenga imani katika ulimwengu wa dijitali ni muhimu sana." Kwa kuwekeza katika hatua za usalama wa mtandao zenye nguvu, Tanzania inaweza kulinda miundombinu yake ya dijitali, kulinda taarifa za kibinafsi, na kukuza uchumi wa kidijiti unaofanikiwa.
Kulingana na ripoti ya Usalama Mtandaoni ya mwaka 2024 iliyotolewa Septemba mwaka huu Tanzania inaongoza nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika kwa kuwa na viwango vya usimamizi vya juu vya Usalama Mitandaoni.
Ripoti hiyo inaonesha Tanzania kuwa na viwango vya juu vya mfano katika ufanisi wa kusimamia nguzo tano za usalama mitandaoni ziliyowekwa na Shirika la Mawasiliano Dunia (ITU) kuanzia mwaka 2015.
Shirika hilo kwa kutambua umuhimu wa kujenga mtandao unaoaminika, jumuishi na salama kwa watumiaji, miundombinu, taarifa za binafsi, na kukuza uchumi wa kidijiti unaofanikiwa. Ilianzisha vigeto ambavyo kila nchi mwanachama itapaswa kufikia ili kufikia hali hiyo. Hiyo ndio ilipekea kuanzishwa ripoti hii maalumu yenye dhumuni la kuzipima hatua za nchi katika vigezo hivyo vilivyo wekwa kwenye nguzo tano.
Nguzo tano zinazopimwa kwenye ripoti hiyo, inayojulikana kama ITU GCIv5 -2024, kifupisho cha jina lake kwa Kiingereza, ni hatua za Kisheria na Ujenzi wa uwezo katika masuala ya Usalama Mtandaoni. Nyingine ni Mipango na Mikakati ya Kiufundi, Mfumo wa Usimamizi na Mashirikiano ya Usalama Mtandaoni.
Mafanikio ya Tanzania yalikuwa asilimia 100 kwenye nguzo ya Sheria, Mifumo ya usimamizi na Ushirikiano; na asilimia 99 kwenye nguzo ya Ufundi na Kujenga uwezo.
Baadhi ya vitu vilivyochangia kupaa kwa Tanzania kwenye CGI ya 2024 ni uwepo wa Mkakati wa Kitaifa wa Usalama Mtandaoni, Sheria na Kanuni za Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi 2022 , na Sheria ya Makosa ya Kimtandao 2015, Kanuni za Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta (CERT) za 2018 na maboresho yake ya 2023 na Timu ya kitaifa ya Mwitikio wa Kukabiliana na Majanga ya Kompyuta (TZ-CERT) timu iliyopo ndani ya muundo wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Timu za Kisekta (GSoC ndani ya e-GA na TZ-FINCERT inayosimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania).
Ushirikiano wa wadau ndani ya nchi, kikanda na kimataifa pia umechangia kwa kiasi kikubwa kuiwezesha Tanzania kufanikiwa katika mchakato huu.
Akihojiwa jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt Jabiri K. Bakari amesisitiza azma ya taasisi yake kama mwanachama wa Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU) kwa niaba ya taifa kuendeleza dhamira ya kitaifa katika masuala ya Usalama na uimara wa mtandao nchini. TCRA itaendelea kushirikiana na taasisi nyingine za wazawa, kikanda na kimataifa.
Ripoti ya GCI ilianza kutolewa mwaka 2015 na Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU)–taasisi ya Umoja wa Mataifa inayosimamia masuala ya Mawasiliano.
A digest of Tanzania Computer Emergency Response Team coverage of cyber-security news across the globe.